Saturday, June 2, 2012

RAIS KIKWETE HATEMBELEWA LEO IKULU NA MMILIKI WA KLABU YA PORTMOUTH Dkt.AL FAHIM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Royal Group ya Saudi Arabia, Dkt. Sulaiman Al Fahim wakati walipokutana leo, Jumamosi, Juni 2, 2012, Ikulu Dar es Salaam. Dkt. Al Fahim ambaye ni mwenyekiti wa zamani na mmiliki mwenza wa Klabu ya soka ya Portsmouth ya Uingereza yuko nchini kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika uchumi wa Tanzania. Dkt. Al Fahim pia ndiye aliyeongoza mazungumzo na kununuliwa kwa klabu bingwa ya Ligi Kuu ya Uingereza ya Manchester City na Kampuni ya Arabuni
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mzungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Royal Group ya Saudi Arabia, Dkt. Sulaiman Al Fahim
.   Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Royal Group ya Saudi Arabia, Dkt. Sulaiman Al Fahim mara baada ya  mazungumzo yao Ikulu leo

HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 01 Juni, 2012

Ndugu Wananchi,

Kama ilivyo ada, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uhai na kutuwezesha kumaliza mwezi Mei salama.  Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza kwa njia hii kila mwisho wa mwezi, leo nitazungumzia mambo matatu. 

Mkutano wa G-8
Jambo la kwanza, ni suala la usalama wa chakula na lishe.  Duniani, inakadiriwa kuwa kuna watu milioni 925 wanaokabiliwa na njaa na lishe duni.  Kati ya hao Afrika ina watu milioni 239 ambao ni karibu theluthi moja ya watu wote wenye tatizo la njaa na lishe duni kote duniani.  Nchi za Afrika zenye tatizo la njaa kiasi cha kuhitaji msaada wa chakula kutoka nje ni 27.  Kati ya hizo 11 zina matatizo makubwa zaidi. Tanzania siyo miongoni mwa nchi hizo, hata hivyo bado hatujafikia kiwango cha kujitosheleza kabisa.  Hivi sasa tumefikia asilimia 95 na kila mwaka yapo maeneo nchini yanayopata msaada wa chakula kutoka Serikalini.  
    
Mwaka 2009, katika mkutano wao wa L’Aquila, Italia, viongozi wa nchi nane tajiri kuliko zote duniani waliamua kuchukua hatua ya kuzisaidia nchi zinazoendelea duniani  kukabiliana na tatizo la njaa na lishe duni.  Katika mkutano ule waliahidi kutoa dola za Marekani  bilioni 22 kwa ajili hiyo.  Tanzania tunategemea kupata dola milioni 22.9.
    
Katika mkutano wa nchi hizo maarufu kwa jina la G-8 uliofanyika Camp David, Marekani tarehe 19 Mei, 2012, pamoja na mambo mengine walizungumzia suala la usalama wa chakula na lishe barani Afrika.  Nia yao ni kuchangia katika juhudi zinazofanywa na mataifa ya Afrika zenye shabaha ya kutokomeza matatizo hayo.  Tofauti na walivyofanya L’Aquila, safari hii waliamua kuchangia katika utekelezaji wa mipango na progamu za kuendeleza kilimo katika nchi za Afrika hasa zile zinazolenga kujenga usalama wa chakula na lishe. 
    
Aidha, waliamua kuwa wataanza na nchi tatu na kuendelea kuziongeza kila baada ya muda fulani, badala ya kuanza na nchi zote mara moja.  Hoja yao kubwa ni kwamba, wanataka kukusanya nguvu zao kwa nchi hizo chache ili kufanya kazi ambayo itakuwa na matokeo yanayoonekana katika kutokomeza njaa na kuboresha lishe.  Hawakupenda kusambaza nguvu zao kwa nchi nyingi na kuishia kutokufanya kazi ya maana. 

Ndugu wananchi;
Bahati nzuri katika programu na mipango ya nchi iliyokubaliwa kwa awamu ya kwanza ni Tanzania, Ethiopia na Ghana.  Na, jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba mpango wetu wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa Kusini mwa Tanzania ulichukuliwa kuwa ni wa mfano.  Maoni hayo ya nchi za G-8 ndiyo maoni ya WEF, Sekretariat ya NEPAD na Umoja wa Afrika, wote wameona kuwa mpango wetu unafaa kuenezwa barani Afrika kama mkakati sahihi wa kuendeleza kilimo, kujitosheleza kwa chakula na kupunguza umaskini.
    
Katika Bara la Afrika mkakati huo sasa unaitwa Grow Africa Partnership na tayari nchi saba zimeshajiunga nao.  Nchi hizo ni Tanzania, Msumbiji, Kenya, Rwanda, Ethiopia, Ghana na Burkina Faso.
Katika mkutano wa Camp David, nchi za Marekani, Japani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Urusi zimeahidi kuchangia nchi yetu katika juhudi zetu za kuendeleza kilimo na hasa zile zenye lengo la kujitosheleza kwa chakula na kuboresha lishe nchini.  Ukichanganya na ahadi iliyotolewa na Umoja wa Ulaya katika mkutano huo, kiasi cha dola za Marekani milioni 897 zimeahidiwa kutolewa kwa nchi yetu kati ya sasa na mwaka 2015. 

Ndugu Wananchi;
Mwaka 2006 tulizindua Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo nchini maarufu kwa kifupi kama ASDP.  Kwa kirefu kwa lugha ya Kiingereza ni the Agricultural Sector Development Programme.  Programu hii ndiyo mwanzo wa safari yetu ya uhakika ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini Tanzania.  Jambo la kwanza lililofanyika katika utayarishaji wa Programu hii ni kutambua vikwazo vinavyozuia maendeleo ya kilimo nchini na kupendekeza hatua za kuchukua za kuondosha vikwazo hivyo.
    
Mwaka 2008, katika tathmini iliyofanywa kwa ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi kwa uamuzi wa Baraza la Biashara Tanzania, ilidhihirika kwamba sekta binafsi ambayo ni wadau muhimu, haijahusishwa vya kutosha katika mikakati, mipango na programu za kuendeleza kilimo nchini.  Kwa pamoja ilikubaliwa kuwa kasoro hiyo iondolewe ili wadau wote washirikishwe, yaani Serikali, wakulima wadogo, wakulima wakubwa na sekta binafsi.  Vilevile, sote tulikubaliana kutoa kipaumbele cha juu kwa maendeleo ya kilimo.  Kwa pamoja tuliafikiana kuwa mambo mengine yanaweza kusubiri isipokuwa kilimo.  Matokeo ya maelewano hayo ndiyo yaliyozaa mkakati na kauli mbiu ya “Kilimo Kwanza”.

Ndugu Wananchi;
Tangu wakati huo, sekta binafsi nchini imekuwa inahusishwa na kushirikishwa kwa karibu katika utekelezajiwa ASDP na kuendeleza kilimo kwa jumla.  Kwa upande mmoja sekta binafsi imekuwa inahusishwa katika upatikanaji wa zana na pembejeo za kisasa za kilimo kwa wakulima.  Kwa ajili hiyo, wenzetu wa sekta binafsi wamekuwa wanategemewa kuleta  na kuuza matrekta, mitambo na vifaa mbalimbali vya kilimo pamoja na mbegu, mbolea, dawa za kuua wadudu waharibifu wa mazao na za kukinga na kutibu maradhi ya mimea na mifugo.  Hali kadhalika, wamekuwa wanajihusisha na ununuzi na usindikaji wa mazao ya mkulima na kuongeza thamani.  Tunataka tuachane na kuendelea kuuza nje mazao ya kilimo kama malighafi na kununua bidhaa zilizotengenezwa na mazao hayo. 
    
Upande mwingine tuliwategemea wenzetu wa sekta binafsi washiriki kulima mashamba makubwa.  Wasiache kazi ya kilimo kufanywa na wakulima wadogo peke yao ambao uwezo wao si mkubwa wa kukabili matatizo ya kuongeza tija.  Nafurahi kwamba wito wangu huo waliupokea vizuri na baadhi yao wameshaanza kufanya hivyo.
    
    
Ndugu Wananchi;
Swali kubwa walilouliza ndugu zetu hao siku ile ya tarehe 2 – 3 Juni, 2009 pale Kunduchi Beach Hotel ni kuhusu upatikanaji wa ardhi.  Niliwaeleza kuwa upo utaratibu mzuri wa kuwapatia wakulima wakubwa ardhi ya kilimo na ufugaji.  Utaratibu wenyewe ni kwamba kila wilaya imetakiwa kutenga ardhi kwa ajili ya wakulima wakubwa.  Hilo likishafanyika, taarifa hutolewa kwa Kituo cha Uwekezaji na kuingizwa katika kitu kinachoitwa Benki ya Ardhi.  Mwekezaji anapojitokeza, kulingana na aina ya kilimo anachotaka kujihusisha nacho, hugawiwa ardhi hiyo.  Ardhi hiyo ni ile ambayo siyo inayotumiwa na wakulima wadogo.  Katu hawanyang’anywi ardhi wakulima wadogo ili kuwapa wakulima wakubwa.  Hiyo  siyo sera wala madhumuni na malengo ya ASDP au Kilimo Kwanza.
Nalifafanua hili kuondoa hofu iliyokuwepo na upotoshaji uliokuwa unafanywa makusudi wa kuhusisha wakulima wakubwa na uporaji wa ardhi.  Siyo makusudio yake hata kidogo. 
    
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2010 tukapanua wigo wa ushiriki wa sekta binafsi kwa kuihusisha sekta binafsi ya kutoka nje ya nchi.  Mwaka huo pia, tukaamua kuipa sekta binafsi lengo maalum la kutekeleza nalo ni kushiriki katika kilimo cha kuhakikisha kuwa nchi yetu inajitosheleza kwa chakula na kupata ziada kubwa ya kuuza nje, kwa majirani zetu na kwingineko.  Shabaha yetu hasa ilikuwa ni kujitosheleza kwa vyakula vikuu vya mahindi, mchele na sukari.
    
Aidha, tuliamua pia kuwa, kwa kuanzia tuelekeze nguvu zetu kwenye mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Iringa na Morogoro kwa vile  mikoa hiyo ndiyo ghala la chakula la nchi yetu. Kwa vile mikoa hiyo ipo ukanda wa kusini ndio maana ikaja kuitwa Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania au SAGCOT.   Tumeamua tukusanye nguvu za Serikali, wakulima, sekta binafsi na washirika wetu wa maendeleo kuwekeza katika kuendeleza kilimo katika mikoa hiyo. 

Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mpango wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa SAGCOT una shabaha kuu mbili: Kwanza kabisa mpango unalenga kuboresha kilimo cha wakulima wadogo ili kitoke kuwa duni na cha kujikimu na kuwa cha kisasa na kibiashara.  Chini ya mpango huu wakulima wadogo watasaidiwa na kuwezeshwa kupata na kutumia zana na pembejeo za kisasa za kilimo.  Pia watawezeshwa kupata mikopo kwa ajili ya kilimo na masoko ya uhakika na yenye bei nzuri kwa mazao yao.  Vile vile, huduma muhimu zitaimarishwa.  Hapa tunazungumzia maafisa ugani na miundombinu ya umwagiliaji, barabara, umeme, maji safi na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Pili, kwa pale inapowezekana kwa maana ya upatikanaji wa ardhi na aina ya mazao, kuihusisha sekta binafsi katika kilimo.  Tayari utekelezaji wa mpango wa SAGCOT umeanza.  Kamati ya Utendaji imeshaundwa na Sekretariati yake imeshateuliwa.  Aidha, Mfuko wa Kuchochea Uwekezaji umeshaanzishwa na unaendelea kuchangiwa fedha.

Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa malengo ya SAGCOT kwa kilimo cha mpunga na kuongeza uzalishaji wa sukari yameanza kutekelezwa.  Matayarisho yanaendelea kwa kilimo cha mahindi na mazao mengine.

Mpango huu utakapofanikiwa utakuwa na manufaa makubwa.  Nchi yetu itajitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada kubwa ya kuuza nje.  Inakadiriwa kuwa mapato yatokanayo na kilimo katika ukanda huu yatafikia dola bilioni 1.2 kwa mwaka, watu 420,000 watapata ajira na watu 2,000,000 wataondokana na umaskini uliokithiri. 

Uwekezaji wake ni mkubwa na kwamba kiasi cha dola bilioni 3.4 kinahitajika kwa kipindi cha miaka 20.  Kwa ushirikiano uliopo baina ya Serikali, sekta binafsi na wabia wetu wa maendeleo wakiwemo wa nchi za G-8, hayo yote yanawezekana.

Ndugu Wananchi;
Tukijitosheleza kwa chakula na kwa maana pana ya chakula chenye lishe bora tutakuwa tumefanikiwa kupata ufumbuzi wa tatizo kubwa la ukosefu wa lishe bora miongoni mwa wananchi wa Tanzania.  Wanaoathirika sana na tatizo hili ni kina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.  Ukosefu wa lishe bora huchangia asilimia 20 ya vifo vya kinamama wajawazito nchini na theluthi moja ya watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.  Aidha, asilimia 42 ya watoto wa umri wa chini ya miaka mitano wamedumaa na asilimia 16 wana uzito mdogo kulingana na umri wao na asilimia 59 wana upungufu wa damu.  Kwa kina mama wajawazito asilimia 41 wana matatizo ya upungufu wa damu.  Hali hii sio nzuri hata kidogo lazima tuibadili na tunaweza kufanya hivyo. Tunao mkakati wa kitaifa wa kuboresha lishe ambao kwa sehemu kubwa utanufaika sana na kufanikiwa kwa mkakati wa  kujitosheleza kwa chakula.

Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
Ndugu Wananchi;
Jana tarehe 31 Mei, 2012 nilishiriki katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa 47 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Mkutano wa 38 wa Mfuko wa Maendeleo wa Afrika.  Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Benki hii tangu ianzishwe mwaka 1964 kwa nchi yetu kuwa mwenyeji wa mikutano hii inayofanyika kila mwaka.  Ni heshima kubwa sana kwa nchi yetu, nami kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote, nimemshukuru sana Rais wa Benki hiyo, Dkt. Donald Kaberuka kwa ihsani kubwa aliyoifanyia nchi yetu.
    
Kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu ni jambo lenye manufaa mengi kwetu.  Kwanza husaidia kuitangaza nchi yetu Barani Afrika na kwingineko duniani.  Pili, ni fursa nzuri ya kuzungumza na viongozi wa Benki kuhusu mipango na miradi yetu ya maendeleo tunayohitaji msaada kutoka Benki hiyo. 

Na, tatu, ni fursa nzuri ya watu wetu kufanya biashara.  Mkutano huu umeshirikisha watu 2,500 ambao wametoka nje ya Tanzania na wanajitegemea kwa kila kitu.  Wenye hoteli, migahawa, vyombo vya usafiri, huduma ya simu, internet na nyinginezo watakuwa wamefanya biashara nzuri katika wiki nzima kabla ya tarehe 28 Mei mkutano ulipoanza hadi 2 Juni, mkutano utakapofungwa. Ni kutokana na manufaa kama haya, ndio maana huwa tunahangaika kuvutia mikutano mikubwa kuja kufanyikia hapa nchini.
    
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa ndugu zetu wa Arusha kwa kuwapokea vizuri na kuwakarimu vyema wageni wetu hao.  Nawaomba waendelee na moyo huo mpaka watakapoondoka wote.  Naomba kuwepo kwa mkutano huu kuwakumbushe umuhimu wa mji wenu kuwa tulivu.  Miaka miwili iliyopita isingekuwa rahisi kwa watu au shirika kubwa la kimataifa kama Benki hii kuamua kufanya mkutano wake Arusha.  Isitoshe hata sisi wenyewe tusingeshawishika kuomba au kukubali maombi ya namna hiyo.  Lakini sasa imewezekana.  Naomba kila mmoja wetu aweke azimio moyoni mwake la kuhakikisha kuwa hali ile haijirudii tena.  Nyota ya Geneva ya Afrika lazima iendelee kuangaza. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

Watanzania Wenzangu;
Niruhusuni tena niwashukuru wenzetu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa mchango mkubwa waliotoa na wanaoendelea kutoa kuchangia maendeleo ya nchi yetu.  Kwa miaka mingi Benki hii imekuwa inatupatia mikopo na misaada muhimu kwa maendeleo ya sekta mbalimbali nchini pamoja na zile za elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara, reli, umeme n.k.

Kwa msaada wa Benki hii tunajenga barabara ya Namanga – Arusha, Minjingu – Singida, Namtumbo – Tunduru, Iringa – Dodoma, Mayamaya – Babati, na Tunduru – Mangaka – Mtambaswala.    Miaka ya nyuma pia walituwezesha kujenga barabara ya Mutukula – Muhutwe.  Aidha, hivi sasa wanagharamia upembuzi yakinifu na usanifu wa reli mpya tunayotaka kuijenga kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda na Burundi.
   
Matukio ya Uvunjifu wa Amani Zanzibar
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni matukio ya wiki iliyopita huko kwenye Jiji la Zanzibar katika mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.  Kama tujuavyo sote kulitokea ghasia zilizochochewa na viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu maarufu kwa jina la Uamsho.  Taasisi hii imeanzishwa kwa madhumuni ya kidini, lakini hivi sasa viongozi wake wameamua kuyaacha madhumuni hayo na kubeba ajenda za siasa.

Siku za nyuma, ndugu zetu hawa walikuwa wakitumia muda mwingi kuilaumu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa lawama hizo sasa hazisikiki.  Lakini, mara tulipoanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mihadhara yao imeelekezwa kupinga Muungano na kuwakashifu viongozi  waasisi wa Muungano na hata waliopo sasa.  Isitoshe wamekuwa wakipandikiza chuki dhidi ya ndugu zao wa kutoka Tanzania Bara na wale wafuasi wa dini ya Kikristo.

Baya zaidi, katika uchochezi huo majengo na mali za Makanisa mawili  zilichomwa moto, maduka ya watu kuvunjwa na mali zao kuibiwa.  Kwa kweli vitendo hivi ni uhalifu ambao haukubaliki na wala hauvumiliki.  Naungana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kauli yake aliyoitoa jana katika mkutano wake na waandishi wa habari ya kukemea vikali na kulaani uhalifu huo. 

Ndugu Wananchi;
Ni jambo la kusikitisha na kushangaza kwamba, wenzetu hawa wamefanya uhalifu huo kwa hoja ya kupinga Muungano.  Haiwezekani mtu anayepinga Muungano, akaitetea hoja yake kwa kuchoma moto makanisa au kuvunja maduka ya watu na kupora mali zao.   Ukristo haukuingizwa Zanzibar na Muungano, bali ulikuwepo karne kadhaa kabla ya Muungano na wala haukutokea Tanzania Bara. Na kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais Ali Mohamed Shein jana, ukweli ni kwamba, dini ya Kikristo kama ilivyo ya Kiislamu imeenezwa Bara kutokea Zanzibar.  Kanisa kuu la Anglikan Zanzibar lilijengwa kuanzia mwaka 1873 na lile la Katoliki kuanzia 1893 ni miongoni mwa Makanisa makongwe kuliko mengi kama siyo yote kwa upande wa Zanzibar na Bara. 

Katika hotuba yake ya jana, Mheshimiwa Rais, Dkt. Ali Mohamed Shein,pamoja na kueleza kwa ufasaha ukweli huu,  pia alisisitiza suala la haki na uhuru wa Kikatiba wa mtu kuchagua au kubadilisha dini au imani yake.  Katika kutumia uhuru huo, mtu hastahili kuingiliwa au kulazimishwa na mtu yo yote. Hayo pia ndiyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Kwa kweli yanayofanywa na ndugu zetu wa Uamsho ya kuchoma moto makanisa siyo sawa hata kidogo.  Na, wanapoyafanya kwa kisingizio cha Muungano ni jambo lisiloeleweka kabisa na wala halina mantiki.  Labda wenzetu wana lao jambo. 

Ndugu Wananchi;
Jambo lingine la kushangaza zaidi ni kule kutokea vurugu na ghasia hizi dhidi ya Muungano wakati ambapo Serikali imetoa fursa sasa kwa watu kutoa maoni yao kwenye mjadala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.  Kama tujuavyo sote, Tume ya Katiba imekwishaundwa na inajiandaa kupita kote nchini kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba mpya waitakayo.  Kama mtu ana maoni yake kuhusu Muungano, hiyo ndiyo fursa ya kufanya hivyo.  Utaratibu mzuri umewekwa kwa ajili yetu sote, vurugu za nini? 

Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu; 
Mimi sioni sababu ya msingi ya kusababisha kuvurugika kwa  amani kwa jambo ambalo limewekewa utaratibu muafaka wa kulishughulikia. Nawaomba tutumie utaratibu mzuri uliowekwa badala ya kufanya mambo yanayoleta mifarakano katika jamii na  yanayosababisha uvunjifu wa amani na yanaharibu sifa na sura ya Wazanzibari na Watanzania isivyostahili.   

Ndugu zangu,
Haipendezi wala haifurahishi kwa Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya raia wake.  Lakini, kama hapana budi, Serikali lazima ifanye na haitasita kufanya hivyo.  Narudia kuwasihi viongozi na wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho kurejea kwenye madhumuni ya msingi ya jumuiya yao.  Wajiepushe na ajenda za kisiasa na kupandikiza chuki zitakazosababisha mifarakano baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano na baina ya Wakristo na Waislamu. Watanzania ni ndugu na wamekuwa wanaishi pamoja kwa upendo na furaha licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini na maeneo watokako. Kimeharibika kipi hata leo yatokee haya? Aidha nawaomba wenye maoni kuhusu Muungano wetu, muundo wake na uendeshaji wake watumie fursa ya mjadala wa Katiba kutoa maoni yao.  Huhitaji kufanya ghasia kutoa maoni yako!

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia fursa hii pia kuwapa pole wale wote walioathirika na vurugu zilizotokea.  Nawaomba wawe wastahamilivu, hiyo ndiyo mitihani ya maisha. Serikali zetu mbili zitafanya kila lililo kwenye mamlaka yake kuwahakikishia wananchi wote usalama wa maisha yao na wa mali zao. 

Nawapongeza vijana wetu wa Jeshi la Polisi kwa juhudi kubwa waliyoifanya ya kudhibiti hali ambayo mwelekeo wake haukuwa mwema.  Nawaomba waendelee kuwa macho ili watu wasioitakia mema nchi yetu na watu wake wasipate nafasi ya kutuvurugia amani na utulivu wetu.  Naamini tukidumisha utamaduni wetu wa kuheshimiana, kuvumiliana na kuzungumza pale tunapotofautiana hakuna litakaloharibika.  Haya shime tufanye hayo.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!

MBWANA SAMATTA AWA GUMZO HUKO ABDIJAN IVORY COAST

Mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars na TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Mbwana Samatta akisaini vitabu na jezi za mashabiki wa mpira wa miguu nchini Ivory Coast jana mara baada ya mazoezi, mchezaji huyo amekuwa gumzo nchini humo kutokana na uwezo wake uwanjani na huenda pia kutokana na timu anayochezea ya TP Mazembe kwani ni timu ambayo imekuwa ikifanya vizuri sana barani Afrika na Dunia pia kwa upande wa vilabu.

UJUMBE WA MAREKANI WAONANA NA RAIS DK. SHEIN

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Seneta wa Marekani Christopher
Coons,akiwa na Ujumbe aliofuatana nao  walipofika Ikulu Mjini Zanzibar
leo,kuzungumza na Rais.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Seneta wa Marekani Christopher
Coons,akiwa na Ujumbe aliofuatana nao  walipofika Ikulu Mjini Zanzibar
leo
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Seneta wa Marekani Christopher
Coons,akiwa na Ujumbe aliofuatana nao  walipofika Ikulu Mjini Zanzibar
leo

KIM ATAJA KIKOSI CHA TAIFA STARS KITAKACHOIVAA IVORY COAST LEO

Kocha Kim Poulsen ametaja kikosi cha Taifa Stars ambacho leo (Juni 2 mwaka huu) kitakuwa uwanjani kwenye Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny jijini Abidjan kuivaa Ivory Coast katika mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia.
Amefanya mabadiliko katika nafasi mbili kwenye kikosi ambacho Mei 26 mwaka huu kilicheza mechi ya kujipima nguvu na Malawi (The Flames) iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa suluhu.
Amir Maftah atacheza beki wa kushoto badala ya Waziri Salum wakati Mrisho Ngasa atakuwa mmoja kati ya washambuliaji wa mwisho. Ngasa atacheza nafasi ya Haruna Moshi ambaye hayuko na Stars hapa baada ya kuumia mazoezini siku moja kabla ya safari.
Kikosi kamili cha Taifa Stars ambayo itatumia mfumo wa 4-4-2 ni kima ifuatavyo;
Kipa; Juma Kaseja
Mabeki; Shomari Kapombe, Amir Maftah, Aggrey Morris na Kevin Yondani
Viungo; Shabani Nditi, Salum Abubakari, Frank Domayo na Mwinyi Kazimoto
Washambuliaji; Mbwana Samata na Mrisho Ngasa
Wachezaji wa akiba; Mwadini Ali, Waziri Salum, Juma Nyoso, Erasto Nyoni, John Bocco, Simon Msuva, Jonas Mkude, Christopher Edward na Ramadhan Singano.
Kim amesema kikosi chake kimejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo, na kilichobaki ni kwa wachezaji kudhibitisha maandalizi hayo kwenye dakika 90 za mchezo huo utakaoanza saa 11 kamili jioni (nyumbani itakuwa saa 2 kamili usiku).
Mechi hiyo itaoneshwa moja kwa moja (live) kupitia televisheni ya RTI ambapo itaonekana katika nchi 58 duniani.
Mwamuzi; Slim Jedidi (Tunisia)
Mwamuzi msaidizi namba 1; Bechir Hassani (Tunisia)
Mwamuzi msaidizi namba mbili; Sherif Hassan (Misri)
Mwamuzi wa akiba; Youssef Essrayri (Tunisia)
Mtathmini wa waamuzi; Rachid Medjiba (Algeria)
Kamishna wa mchezo; Saleh Issa Mahamat (Chad)

WATU SABA WALIOITIKISA MICHUANO YA EURO 1984-2008

MICHEL PLATINI (1984)
Mfaransa huyu  kwa sasa anajulikana zaidi kama Raisi wa Uefa mwenye sheria za utata zaidi, lakini hakuna mchezaji aliyeitawala michuano ya 1984 kama yeye.

Kiungo huyu wa aina yake alifunga mabao tisa kwenye mechi tano huku akiiongoza nchi yake kushinda ubingwa wa ulaya kwenye ardhi ya nyumbani.

Baada ya kufunga hat-tricks mbili kwenye mechi za hatua ya makundi, Platini alifunga bao kwenye dakika za nyongeza za mechi ya nusu fainali dhidi ya Ureno.

Ufaransa wakaingia fainali na kwa mara nyingine alifanya balaa kwa kupiga faulo iliyotinga nyavuni kwa kumshinda golikipa wa Spain Luis Arconada.
MARCO VAN BASTEN (1988)
Career ya Mholanzi iliishia njiani kutokana na balaa la majeruhi, lakini huyu jamaa alikuwa kwenye kiwango cha juu sana.

Unless, labda kama ulikuwa muingereza, baada ya timu zote mbili za mataifa haya kufungwa kwenye mechi zao za ufunguzi, mechi ya kundi B kati ya Uholanzi na England ilikuwa muhimu sana.

Van Basten akafunga hat-trickna kumsumbua sana kinda Tony Adams, wakati wadachi walipowafungasha virago England.

Mchezaji bora wa ulaya kwa mara ya tatu alienda na kufunga goli la ushindi la ushindi dhidi ya Ujerumani magharibi kwenye nusu fainali lakini balaa zaidi lilikuwa njiani.

Van alifunga bonge la bao kwenye 'impossible angle' dhidi ya Umoja wa Soviet - goli ambalo linatajwa kama moja ya mabao bora kabisa ya fainali za ulaya.

Alimaliza michuano hiyo kama mfungaji bora.
PETER SCHMEICHEL (1992)
Ulikuwa umepita mwaka mmoja tu tangu Sir Alex Ferguson alipe £505,000 kumnunua mdenmark huyu.

Denmark haikuwa hata ikitakiwa kushiriki michuano hiyo lakini walichukua nafasi ya nchi iliyokuwa kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe Yugoslavia na wakaweza kuwashangaza watu na kubeba ndoo ya ulaya.

Hilo liliwezekana zaidi kutokana na uwezo wa golikipa ambaye alitisha sana kwa kuzuia michomo ya hatari.

Schmeichel aliikoa mpaka penati ya Marco van Basten na kupelekea Uholanzi iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa kutolewa kwenye mashindano katika hatua ya nusu fainali.

Hatari ya Denmark iliendelea huku Schmeichel akitoka na clean sheet kwenye ushindi wa 2-0 kwenye fainali dhidi ya Ujerumani.
ALAN SHEARER (1996)
Kwa kukumbuka kiangazi cha mwaka 1996, mshambuliaji huyu alikuwa akiwafanyia umafia mabeki wa pinzani    - akifunga magoli kutoka kwenye kila angle - alikuwa mshambuliaji wa kati aliyekamilika haswa.

Ndio ni rahisi kusahau kwamba alienda kwenye Euro 96 akiwa hajafunga katika mechi 12 ndani ya 21 akiwa na England.

Ingawa makelele yote aliyokuwa anapigiwa kocha Terry Venables kumtema mshambuliaji yalianza kuisha na kusahaulika mara tu alipofunga goli kwanza kwenye michuano hiyo katika dakika ya 22 dhidi ya Switzerland.

Kutoka pale akaendeleza balaa zaidi. Kwenye mechi dhidi ya Scotland na kabla ya kuwatesa sana Uholanzi kwenye mechi ambayo England iliwakandamiza wadachi 4-1 pale Wembley.

Shearer aliendeleza kufunga mabao katika mechi robo fainali England ikiwatoa Spain kabla ya kuwapa mashabiki wa England mwanzo mzuri alipofunga bao la kuongoza dhidi ya Ujerumani, ingawa England wakatolewa kwa mikwaju ya penati baada ya Gareth Southgate kukosa penati yake.

Shearer alimaliza michuano hiyo kama mfungaji bora na kubeba kiatu cha dhahabu.
ZINEDINE ZIDANE(2000)
Wakati mwingine wa dhahabu wa michuano hii kwa Ufaransa ulihitimishwa na David Trezeguet.
Lakini wakitoka kushinda kombe la dunia miaka miwili nyuma, michuano hiyo iliyofanyika kwenye ardhi za Uholanzi na Ubelgiji ilimpa nafasi Zidane nafasi ya kuweka heshima zaidi kwamba ndio mchezaji bora wa wakati wake.

Wakisikia kelele za mwangi za ushindi wa akina Platini miaka 16 nyuma, Zidane akafunga bao kwenye extra time dhidi ya Ureno katika nusu fainali ya aina yake - kwa mkwaju wa penati.

Zidane alikuwa akitimiza miaka 30 siku tisa kabla ya fainali na akapokea zawadi ya siku ya kuzaliwa kwa kutajwa na UEFA kama mchezaji bora wa michuano hiyo.

OTTO REHHAGEL(2004)
Shujaa aliyekuwa hategemewi, mjerumani, ambaye sasa ana miaka 73, akawa mungu wa soka nchini Ugiriki  baada ya kuiongoza nchi hiyo kwenye kubeba kombe mwaka 2004

Akiwa bingwa wa kuunda ukuta wa kupaki basi golini chini ya nahodha, Theo Zagorakis kutoka Leicester City, Rehhagel alifanya maajabu mwaka 2004.

Aliiongoza timu yake kupita kwenye hatua ya makundi huku wakishinda mechi zote kwa ushindi wa 1-0 - hata ushindi wa fainali dhidi ya Ureno ulikuwa wa goli 1-0 dhidi ya wenyeji.

Siri ya mafanikio? Nyuma ya kila kocha aliyefanikiwa kuna mke mzuri wa kocha huyo na mama watoto wa Otto, Beate, ameripotiwa huwa anaenda kufanya scouting kwa wapinzani kwa ajili ya mumewe.
DAVID VILLA(2008)
Ilikuwa ni michuano ambayo wahispania waliweka heshima baada ya kutaniwa kama warembaji kwa muda mrefu - lakini kipaji cha ajabu cha David Villa kiliiongoza Spain kujenga heshima mpya.

Mshambuliaji wa Valencia tayari alikuwa ameshafunga mabao 6 kwenye hatua ya kufuzu na akafungua michuano kwa kufunga hat-trick dhidi ya Russia.

Huku akiwa anamfunika patna wake mshambuliaji mpya wa Liverpool Fernando Torres, Villa then akafunga goli la muda wa majeruhi katika mchezo wa pili dhidi ya Sweden.

Alipumzishwa kwenye mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi, na akarudi kwenye robo fainali na akafunga bao la penati kwenye hatua ya mikwaju ya penati dhidi ya Italia na kuisadia timu yake kufika nusu fainali.

Alipata maumivu kwenye nusu fainali na akashindwa kupata nafuu kucheza mchezo dhidi ya Ujerumani ambao Fernando Torres akafunga bao la ushindi dhidi ya Ujerumani na kuwapa ubingwa Spain - huku David Villa akiibuka mfungaji bora wa michuano.


JE MWAKA HUU NANI ATAITAWALA  MICHUANO YA 2012.