Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa kwa kitendo
alichofanyiwa Dk. Steven Ulimboka cha kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa
vibaya na watu wasiojulikana kilichotokea tarehe 26 usiku, Juni 2012 na
kukutwa ametupwa katika eneo la Mabwepande lililoko nje kidogo ya jiji
la Dar es Salaam.
Tume
inalaani kitendo hicho cha kinyama kwani kinakwenda kinyume na Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Kifungu cha 12(2)
kinachoitaka jamii kutambua na kuthamini utu wa mtu.
Vile
vile kitendo hicho kinakiuka haki ya msingi ya mtu kutoteswa,
kutoadhibiwa kinyama na kikatili au kudhalilishwa kama inavyoainishwa
katika Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Kifungu cha 5 cha Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu.
Tanzania
ni nchi yenye amani na inayofuata sheria na taratibu zake, hivyo kwa
sababu yoyote ile ni kosa kumteka na kumtendea mtu vitendo vya kinyama
na vya udhalilishaji wa utu wake.
Ili
kuwa na jamii yenye utamaduni ambao unakuza, kulinda na kuheshimu haki
za binadamu na misingi ya utawala bora nchini Tume ya Haki za Binadamu
na Utawala Bora inaamini kuwa haki lazima itendeke na ionekane
kutendeka. Hivyo basi:
1. Tume
inalaani kitendo cha kujichukulia sheria mkononi na matumizi ya nguvu
kilichofanywa na kikundi cha watu waliomteka Dk. Ulimboka;
2. THBUB
inalaani vikali vitendo vilivyofanywa na kikundi au taasisi yoyote
ambacho kimemnyima Dk. Ulimboka haki yake ya kikatiba ya kuheshimiwa utu
wake na kutofanyiwa vitendo vya kinyama na vya kudhalilisha;
3. Tume inatoa wito kwa wananchi na vyombo vya dola kuheshimu sheria, utawala wa sheria, haki za binadamu na utawala bora;
4. Tume
inatoa wito kwa Serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini
waliofanya kitendo hicho cha kinyama, sababu za kufanya kitendo hicho na
kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.
5. Tume
inampa pole sana Dk. Ulimboka na inamuombea kwa Mwenyezi Mungu apate
nafuu ya haraka ili aweze kuendelea na maisha yake ya kawaida.
No comments:
Post a Comment