Saturday, June 30, 2012

Dk KARUME:CCM HAIJALALA,HAITAKI KUAMSHWA

Na Thabit Jaha, Zanzibar
Hatimaye Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk Amani Abeid Karume leo amejitokeza hadharani na kuwataka wanaCCM kutobabika na watu wanaotoa maoni yao kuhusu muundo wa Muungano uliopo.
Dk Karume alitoa matamshi hayo wakati akizungumza na wanachama wa matawi mawili ya Mwembeladu na Gulioni leo mjini hapa.
Alisema wote wanaotoa maoni kimsingi wanatumia haki yao ya kiraia na kiemokrasia hivyo wanaCCM wanachotakiwa ni kuendelea kusimamia ujenzi wa chama chao na kuheshimu misimamo yao bila ya kuyumbishwa.
“Kwani nyie mmelala usingizi?, basi iweje msihofie kuamshwa, la muhimu kwenu ni kujipanga na kukijenga chama chenu ili kiendellee kushinda uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015’ Alisisitiza Dk Karume
Dk Karume aliwataka wanachama wenzake hao kuongeza kasi ya kuzieneza sera za CCM ndani ya umma ili kuzidi kuwavutia wanachama wapya kujiunga na chama hicho.
Rais huyo mstaafu wa Zanzibar alisema kuwa katika hoja ya Muungano wako baadhi ya watu wanaotaka Muungano uendelee,wengine wakitaka ufanyiwe marekebisho na mabadiliko na wengine wakitaka uvunjike.
“Msipatwe na homa, ondoeni hofu na wqsiwasi , acheni masheikh wajibishane na mashekh wenzao na sisi wanasiasa tutafute majibu yatakayofaa ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha vijana wetu kutambua mahali tulikotoka, tulipo sasa na kule tuendako”Alisema.
Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alitamka bayana kuwakatika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa njia pekee ni kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura ili kushinda katika kila uchaguzi na si kinyume chake.
Aidha Dk Karume aliwaeleza wanachama hao wa CCM  kuwa chama chao ndicho kilichosaka amani iliopo hivi sasa Zanzibar  baada ya mataifa nya nje ,nchi wahisani na jumuiya za kimataifa kushindwa kuleta suluhu tokea mwaka 1995.
“Tumesaka muafaka mara tatu bila mafanikio, baadhi ya wenzetu wakajifungia kwa miaezi 18 huko Bagamoyo nao hawakupa suluhisho, sasa tuna amani ,na Zanzibar imetulia kama maji ndani ya mtungi"Alisema
Pia Dk Karume aliwakumbusha wanaCCM wenzake kuwa pamoja na kupata shinikizo toka mataifa ya nje ilishindika kufikia muafaka wa kudumu ila kutokana na sera ya CCM kuhimiza amani, umoja na maendeleo hatimae sasa maridhiano ya kisiasa yakapatikana.

No comments:

Post a Comment