Friday, June 1, 2012

MAUZAUZA YAENDELEA KWENYE SOKA LA BONGO

Wakati klabu ya Simba ikiwa imejihakikishia kukamilisha usajili wa kinda la Azam under 20, Ibrahimu Jeba ambaye leo hii asubuhi alionekana kwenye mazoezi ya gym ya Simba - maeneo ya Chang'ombe. Uongozi wa klabu ya Azam FC umesema Simba inajidanganya kuhusu kumsajili mchezaji huyo ambaye Azam walimpeleka Villa Squad kwa mkopo kwa kujifua zaidi msimu uliopita.
Meneja wa klabu ya Azam FC, Patrick Kahemele amesema mabingwa wa Tanzania bara wanafanya uhuni kwenye uhamisho wa mchezaji huyo ambaye bado ana mkataba na klabu hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara Salim Bakheresa. "Simba wanafanya uhuni katika hili kama ilivyo kawaida yao, Jeba ni mchezaji wetu halali na bado ana mkataba na Azam. Kumbukumbu sahihi nilizonazo ni kwamba Ibrahimu Jeba alisaini mkataba wa kuichezea Azam kwa miaka miwili mwezi Desemba 2011 na akachukua kiasi cha fedha kama ada ya usajili - kabla ya kuelekezwa kwamba akacheze Villa Squad kwa mkopo ili apate nafasi ya kujifua then msimu huu arudi Azam FC. Simba wakaenda wakamrubuni asicheze Villa, na Jeba bado mdogo hivyo ikawa rahisi kumrubuni, na Azam hatukutaka kufanya nao malumbano kwa sababu suala hilo tayari tuna mkataba ambao umesajiliwa kabisa na TFF, ambao walishatuambia haki zetu za msingi zitalindwa."


Kahemele alipoulizwa ikiwa Simba wanataka kulimaliza hilo suala itabidi walipe kiasi gani alijibu, "Kiukweli sie tulishatangaza mapema kwamba hakuna mchezaji yoyote ambaye ameachwa wala yupo sokoni kwa msimu ujao. Hivyo kama Simba wanamtaka Ibrahimu Jeba kihalali basi atawagharimu sana kwa kuwa sisi tunamuona Jeba akiwa na thamani ya Shilingi millioni 50 na uwachanganye wachezaji wawili wa Simba Jonas Mkude na Shomari Kapombe, then hapo tunaweza kuwafikiria kuwaachia Jeba vinginevyo haitowezekana Jeba kuichezea klabu yao."

No comments:

Post a Comment